Alhamisi, 7 Mei 2015

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue azindua timu ya wataalam wa serikali wa kufanya mazungumzo katika mikataba ya gesi asilia na mafuta


  Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akizungumza wakati wa kuzindua timu ya wataalam wa mazungumzo katika mikataba ya gesi na mafuta kutoka serikalini na mafunzo yao maalum yaliyofanyika katika hoteli ya Park Hyatt kisiwani Zanzibar jana. Kutoka kulia ni Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk. Abdulhamid Yahya Mzee na Bi. Sheila Khama Mkurugenzi wa Kituo cha Rasilimali za Afrika katika Benki ya Maendeleo ya Afrika. 
 Afisa Mtendaji Mkuu wa UONGOZI Institute Profesa Joseph Semboja akitoa hotuba ya kumkaribisha mgeni rasmi na wageni waalikwa katika uzinduzi wa timu hiyo ya wataalam wa mazungumzo katika mikataba ya gesi na mafuta ambao umeenda sambamba na mafunzo maalum ya siku mbili kisiwani Zanzibar. UONGOZI Institute ikishirikiana na Chuo Kikuu cha Columbia (Taasisi ya Uwekezaji Endelevu) na Mradi wa Wanasheria Waandamizi wa Kimataifa ndio waandaji wakuu wa timu hiyo ya wataalam ambao watapitia mafunzo ya miezi sita katika masuala ya yatakayowanoa kupata mikataba bora ya mafuta na gesi asilia kwa manufaa bora ya nchi. 
 Taswira ya wageni waalikwa pamoja na washiriki wa mafunzo ya wataalam wa mazungumzo katika mikataba ya gesi na mafuta. Wataalam ishirini na tano waliochaguliwa kuingia katika timu ya mazungumzo wanatoka katika ofisi na taasisi mbali mbali kama Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Fedha, Wizara ya Kazi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, TANESCO, TPDC, Tume ya Mipango, STAMICO, Ofisi ya Waziri Mkuu, Benki Kuu, TRA, Wizara ya Viwanda na Biashara, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, TAMISEMI na NEMC.
Mjadala wa mafuta na gesi ukiendelea. 



Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania leo imezindua timu ya wataalam ambao wamechaguliwa kwa ajili ya kuwakilisha serikali katika mazungumzo ya mikataba ya gesi asilia na mafuta na kampuni za kimataifa ya gesi asilia na mafuta ili kuweza kuleta mikataba yenye manufaa makubwa kijamii na kiuchumi kwa ajili ya taifa la Tanzania na watu wake kwa ujumla. 

 Timu hii ya wataalam inajumuisha watu 25 wenye utaalam mbali mbali waliochukuliwa kutoka ofisi na taasisi tofauti za serikali ili kuhakikisha kwamba masuala katika uchumi endelevu wa gesi na mafuta yanatatuliwa ipasavyo. Wataalam hao wametoka katika ofisi na taasisi mbali mbali kama Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Fedha, Wizara ya Kazi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, TANESCO, TPDC, Tume ya Mipango, STAMICO, Ofisi ya Waziri Mkuu, Benki Kuu, TRA, Wizara ya Viwanda na Biashara, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, TAMISEMI na NEMC. 

Akizindua timu hiyo ya wataalam wa mazungumzo ya mikataba ya gesi asilia na mafuta kutoka serikalini iliyoenda sambamba na mafunzo ya mazungumzo ya awali ya siku mbili iliyoandaliwa na Taasisi ya Uongozi Afrika kwa Maendeleo Endelevu (UONGOZI Institute) katika Hoteli ya Park Hyatt kisiwani Zanzibar, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue alisema  kwamba mpango huo itawawezesha kuwapatia wataalam wa kufanya mazungumzo yenye ueledi na mafanikio kwa taifa. 

 “Ni matumaini yangu kwamba mafunzo haya yatawawezesha wahusika kuweza kupata ujuzi na umahiri wa kutosha kufanya mazungumzo yatakayoleta manufaa makubwa kwa ajili ya taifa letu sasa na kwa ajili ya vizazi vijavyo pia,” alisema. Balozi Sefue aliwashauri pia hii timu mpya ya wataalam .

“kujitolea kujifunza, kuelewa, kufikiria kimkakati, kusimamia, kutafiti, kuchunguza na muhimu zaidi kufanya mazungumzo vizuri kwa niaba yetu wote, kwa ajili ya maslahi ya Tanzania kwa sasa na hata baadaye.” Balozi Sefue aliendelea, 

“Kufanya mazungumzo ya mikataba ya mafuta na gesi asilia na kampuni za kimataifa ya mafuta ni changamoto kubwa kwa serikali za nchi zilizobarikiwa na rasilimali nyingi kutoka Afrika, changamoto ambayo lazima itatuliwe.” Balozi Sefue alisema kwamba kampuni hizi za kimataifa za mafuta zinauwezo mkubwa wa kuleta wataalam wao waliobobea katika fani za uhandisi, kiuchumi na kisheria kutoka duniani kote na wenye uzoefu wa muda mrefu sana. 
Kwahiyo, changamoto ya kwanza kabisa ambayo serikali za Afrika inakumbana nayo ni hii ya kutokuwa na wataalam wenye uwezo wa kutosha ukilinganisha na kampuni za kimataifa ya mafuta na gesi asilia. 

 Aliongeza, “Tayari ugunduzi wa futi za ujazo trilioni 50 za gesi asilia zinaweza na inapaswa kuleta chachu ya kufanya mageuzi ya kiuchumi katika nchi yetu ili iweze kuwa nchi endelevu yenye kipato cha kati katika miaka ya hivi karibuni. Lakini ili hii ifanyike, tunapaswa kuiga yale mazuri, kutokurudia makosa ambayo nchi zingine wamekwisha yafanya huko nyuma na pia inatubidi tufanye mazungumzo mazuri ili kupata mikataba bora.” 

Balozi Sefue aliwasihi timu hiyo ya wataalam kupitia na kuelewa jitihada za serikali zilizokwisha fanyika huko nyuma na zinazoendelea ili kuweza kupata muundo mzuri wa jinsi ya kusimamia vizuri sekta hii ya mafuta na gesi asilia. “Kwa mfano kuna mengi ambayo yamefanywa kama kutengeneza sera, mikakati na sheria, na zote hizi lazima zieleweke na zizingatiwe katika mafunzo yenu na mazungumzo mtakayokwenda kuyafanya,” alisema.
Aliongeza, “Itabidi wataalam wetu wajiandae vizuri kwa ajili ya kufanya mazungumzo yenye ueledi mkubwa itakayo kuwa na malengo ya kuleta usawa katika pande zote mbili wa serikali na kampuni za kimataifa ya gesi asilia na mafuta.” 

Kutokana na maelezo ya Katibu Mkuu Kiongozi kuna umuhimu wa kufanya mipango kwa ajili ya kufikia aina ya taifa tunayoitaka. Kama hatutakuwa na maamuzi ya kimkakati na ambayo yatafanywa katika hatua hizi za awali, kutakuwa na hatari ya kutokea kwa matabaka ya kiuchumi na kijamii na mwishowe kuzaa laana ya rasilimali. 

 “Lazima tuepukane na laana ya rasilimali ambazo nchi zingine zimesha tumbukiza humo. Serikali ya Tanzania imedhamiria kwamba uwepo wa gesi asilia lazima iwezeshe mageuzi ya kijamii na kichumi kwa ajili ya kuifanya nchi yetu kuwa ya kipato cha kati na ukuaji endelevu na mpana kwa manufaa ya wengi na maendeleo ya watu wote kama ilivyoainishwa katika dira ya maendeleo ya Tanzania ya 2025.”

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni